Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje

Mamlaka ya  Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje

Karibu

Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) ilianzishwa Februari, 2006 kwa marekebisho ya Sheria ya EPZ numba 11 ya mwaka 2002. Mamlaka inafanya kazi zake chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. EPZA inasimamia programu mbili za uwekezaji, Export Processing Zone (EPZ) na Special Economic Zone (SEZ) Programu ya EPZ ilianzishwa kwa Sheria namba 11 ya mwaka 2002 ambapo awali, jukumu la utekelezaji wa EPZ liliwekwa chini ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).

Programu ya SEZ ilianzishwa na Sheria ya SEZ (Special Economic Zone Act) iliyopitishwa mwezi Februari, 2006. SEZ ni Mkakati wa kutekeleza ”Mini-Tiger” Plan 2020 na inalenga kuharakisha Ukuaji wa Uchumi na Kupunguza Umaskini.

EPZ inahusisha uzalishaji wa bidhaa viwandani kwa mauzo ya nje ambao asilimia 80% (au zaidi) ya bidhaa zinazozalishwa lazima ziuzwe nje ya nchi, wakati SEZ inajumuisha sekta zingine zote kama Kilimo, Misitu, Biashara, nk; pia inahusisha mauzo ya nje na ndani ya nchi pasipo kigezo cha kiwango cha asilimia za mauzo.

Mamlaka inatoa leseni za aina tatu kama ifuatavyo;

  1. Leseni ya Ujenzi (SEZ Developer License) ambapo leseni hii ni kwa ajili ya wawekezaji wa kujenga miundombinu ya SEZ/EPZ katika maeneo yaliyobainishwa.
  2. Leseni ya kuanzisha kiwanda (EPZ/SEZ operator License). Leseni hii ni kwa ajili ya wawekezaji wanaozalisha bidhaakatika Maeneo Maalum ya uwekezaji SEZ/EPZ yaliyokamilika kujengwa.
  3. Leseni ya Kutoa Huduma Katika Maeneo Maalum (EPZ/SEZ Service Providers License). Leseni hii ni kwa ajili ya wawekezaji wanaotoa huduma katika maeneo maalum ya uwekezaji, kama maji, umeme, mawasiliano, na huduma za fedha (Benki).

Vilevile uwekezaji katika ujenzi wa EPZ na SEZ upo katika makundi matatu kama ifuatavyo:

  1. Uwekezaji unaofanywa na Serikali asilimia mia moja (Public Sector Investment); mfano Eneo Maalum la Uwekezaji la Benjamin William Mkapa SEZ lililopo Mabibo External, Dar es Salaam.
  2. Uwekezaji kati ya Serikali na Sekta Binafsi (Private Public Partnership). Mfano Eneo la uwekezaji la Bagamoyo SEZ.
  3. Uwekezaji unaofanywa na Sekta Binafsi kwa asilimia mia moja (Private Financing Initiative); Mfano Eneo Maalum la Uwekezaji Star City SEZ lililopo Morogoro.

Hivyo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya EPZ na SEZ kutoka katika makundi hayo, EPZA itabaki kumiliki uwekezaji uliofanywa na Serikali na kutoa mwongozo kwa SEZ za Serikali kuhusiana na uwekezaji wa ubia uliofanywa na sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali.

Kwa Mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 (TDV 2025), na kwa mujibu wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Sekta ya Viwanda ndiyo itakuwa Sekta Kiongozi kwenye Uchumi kwa maana ya kuongeza mchango katika Pato la Taifa, Fedha za Kigeni na kutoa Ajira kwa Watanzania walio wengi. Katika kutekeleza majukumu ya kuendeleza sekta ya Viwanda kuwa Sekta Kiongozi, EPZA inalo jukumu la Kuongoza, Kusimamia na Kuratibu ujenzi wa viwanda katika Maeneo Maalum mbalimbali ya Uwekezaji yaliyobainishwa na Mamlaka

Tunakukaribisha Uwekeze katika Maeneo Maalum ya EPZ na SEZ.

John Mathew Mnali

KAIMU MKURUGENZI MKUU